TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO LA SITA LA JUMUIYA YA TAASISI ZA MITAALA AFRIKA
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji katika Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (African Curriculum Association - ACA) litakalofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 25, Septemba 2026 katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika Kongamano hilo la siku nne anatarajia kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratias John Ndejembi anayetarajia kuambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa na mashirika ya ndani na nje ya nchi.
Akiongea na Waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema, TET kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ) wanakuwa wenyeji wa kongamano hilo litawakutanisha taasisi zinazofanya kazi ya kubuni, kuandaa na kuboresha Mitaala barani Afrika kwa ajili ya kubadilishana maarifa, matokeo ya tafiti, uzoefu na bunifu kuhusu mabadiliko ya mitaala na mifumo ya elimu, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya Afrika na ulimwengu kwa ujumla.
Aidha Dkt. Komba amesema kuwa Kongamano la ACA 2026 litatoa fursa kwa nchi nyingine kujifunza kutoka Tanzania pamoja na kushirikishana uzoefu na nchi nyingine kuhusu mageuzi ya Mitaala yaliyofanyika nchini na kuanza kutekelezwa kuanzia Januari 2024.
“Kongamano hili linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Lengo la 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 4) nyaraka hizi zote zinasisitiza umuhimu wa kutoa elimu bora inayolenga kujenga wahitimu wenye ujuzi na wanaoweza kutumia ujuzi wao kutatua changamoto katika jamii zao,” amesema Dkt. Komba.
Dkt. Komba amesema kuwa Tanzania imekuwa ikishiriki katika makongamano yaliyopita yaliyofanyika katika nchi mbalimbali za Afrika na kwamba kwa sasa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo ni fursa muhimu kwa nchi yetu kuonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika elimu ikiwemo maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023, mfumo ya elimu na mitaala, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka nchi nyingine pamoja na kuchangia katika mwelekeo na maendeleo ya elimu barani Afrika.
Washiriki katika kongamano hili ni wakuza mitaala, watafiti wa elimu, wataalamu na wadau wa mitaala na elimu kwa ujumla kutoka sekta za umma na binafsi, watunga sera, washirika wa maendeleo, watekelezaji wa mitaala wakiwemo walimu na wakufunzi, wahadhirii na wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu katika maswala ya elimu kutoka Tanzania, Afrika na maeneo mengine duniani.