Imewekwa: 28th March, 2023
Wadhibiti
Ubora na Maafisa Elimu Kata wa Halmashauri za wilaya tatu za Mkoa wa Dodoma jana
tarehe 27/3/2023 wameanza mafunzo ya siku tano kwa ajili ya kupata uzoefu wa
utekelezaji wa shughuli za elimu na afya katika kuunda, kusimamia, kutoa
taarifa na kuratibu shughuli za Mradi wa Timiza Malengo.
Akifungua
mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, Dkt. Semestatus Mashimba
amewataka washiriki hao kufuata miongozo
ya ufundishaji, maadili ya Kitanzania pamoja na tamaduni ili kukabiliana na wimbi la mmomonyoko wa maadili.
“Hakikisheni
mnafuatilia vyema mafunzo haya ili mkienda kwenye ufuatiliaji mkasaidie kuondoa
mmomonyoko wa maadili yetu hasa kwa vijana nchini”amesema Dkt. Mashimba.
Mafunzo
hayo yanaendeshwa na Taasisi ya Elimu (TET) na Tume ya Taifa ya Kudhibiti
Ukimwi (TACAIDS) ambapo jumla ya Halmashauri 18 nchi nzima zitafikiwa katika
kuhakikisha elimu hiyo inawafikia
walengwa ambao ni wanafunzi nchini.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala TE, Dkt. Fika Mwakabungu amesema
kuwa mafunzo hayo yatasaidia kukuza uelewa wa pamoja kuhusu elimu ya Stadi za
Maisha zinazolenga Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI na Jinsia, kuwezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa mitaala kwa
kulenga mafunzo yaliyotolewa kwa walimu kuhusu maudhui lengwa katika ngazi ya
darasa.
Pia
watajenga mtazamo chanya katika kuwahamasisha walimu, wanafunzi na vijana
katika jamii kuzingatia misingi ya afya ili kupunguza maambukizi ya magonjwa
kwa ustawi wa nguvu kazi ya vijana.
Aidha,
Mratibu wa Mafunzo wa TACAIDS,Bwana. Kelvin Kisoma amesema kuwa mafunzo hayo
yatasaidia washiriki kuongeza uelewa na kuwa namna bora ya kusimamia,kuratibu
na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maudhui ya stadi za Maisha
inayozingatia afya ya uzazi, VVU na
UKIMWI na ukatili wa kijinsia
Halmashauri
zinazoshiriki mafunzo hayo ni kutoka Mpwapwa,Dodoma jiji na Mpwapwa ambapo
Halmashauri nyingine za Geita na Chato zikitarajia mafunzo
hayo wiki ijayo.