Imewekwa: 31st March, 2023
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) jana tarehe 30/03/2023 imesaini
mkataba wa makubalino ya ushirikiano wa miaka mitatu na Chuo Kikuu cha
Shanghai-Normal cha nchini China katika masuala mbalimbali yanayohusu elimu.
Katika halfa hiyo iliyofanyika katika ofisi za TET Jijini Dar es
salaam, Mthibiti Mkuu wa Shule Kanda ya Dar es Salaam Bi.Zahra Nassor
aliyemwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, amesema kuwa, uhusiano wa nchi hizi katika
masuala ya kielimu utasaidia kubadilishana ujuzi na uzoefu katika kufundisha na
kujifunza somo la Hisabati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba amesema
kuwa,makubaliano hayo yanalenga kukuza na kupanua ushirikiano kati ya Jamhuri ya watu wa China
na Tanzania.
"Kama mnavyojua Tanzania imekuwa ikishirikiana na China katika
masuala mbalimbali yakiwemo ya Kielimu, ujenzi wa miundo mbinu, afya na huduma
nyingine nyingi. Hivyo, ushirikiano huu tunaoenda kutia saini leo utadumisha
ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili. Amesema Dkt.Komba.
Dkt. Komba alieleza kuwa, mkataba huo una malengo ya kukuza ubora wa
Elimu ya msingi hasa Elimu ya Hisabati na Elimu ya Ualimu nchini, kuongeza
ushirikiano kati ya Tanzania na China katika tafiti za kielimu, kukuza uelewa
katika maarifa na ufundishaji wa somo la Hisabati kwa walimu na wanafunzi
Tanzania pamoja na kutoa fursa za kujiendeleza kitaaluma kwa Walimu na Wakuza
Mitaala.
Aidha, Dkt. Komba amesema kuwa, baada ya makubalino haya, TET na
Chuo Kikuu cha Shanghai wataendeleza juhudi za kuendelea kutoa mafunzo kwa
Walimu, Wakufunzi wa Vyuo na Wakuza Mitaala ili kukuza maarifa na uelewa wa
njia na mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Hisabati.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Unesco cha Elimu ya
Ualimu (Unesco-TEC), Prof. HU Guoyong amesema kuwa,ushirikiano huu utakuwa na
manufaa makubwa haswa katika kushirikiana katika kuwajengea uwezo wadau wa
elimu haswa Walimu, Wakufunzi na Wakuza Mitaala.
Prof. Guoyong amebainisha kuwa katika ushirikiano huu, wataalam wa
Hisabati watapata fursa za kubadilishana uzoefu kupitia mafunzo endelevu ya
walimu kazini.