Serikali Yatumia Shilingi Bil 46 Kuchapa Vitabu
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya elimu nchini, imetumia shilingi bilioni 46.476 kwa ajili ya kuchapa nakala 20,943,989 ya vitabu vya elimu kuanzia ngazi ya Awali, Msingi, Kundirika, Maandishi yaliyokuzwa pamoja na Sekondari.
Hayo yamesemwa leo tarehe 15/10/2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Profesa Joyce Ndalichako katika uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vitabu hivyo katika halmashauri zote 184 nchini, kwa uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili.
"Wizara itaendelea kusimamia kila pesa inayoletwa na Serikali katika kuendeleza elimu nchini hivyo napenda kutoa shukrani zangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu" amesema Mhe.Ndalichako.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt Aneth Komba amesema kuwa, vitabu hivyo vimeandaliwa na wataalamu wa TET kwa kushirikiana na wataalamu wengine kutoka vyuo vikuu, vyuo vya ualimu pamoja na walimu kutoka shule za sekondari na msingi.
Zoezi la usambazaji wa vitabu hivyo limeanza leo mara tu baada ya uzinduzi.