SERIKALI KUIWEZESHA TET KUCHAPA VITABU NCHINI
Imewekwa: 15th May, 2022
Serikali imesema itaiwezesha Taasisi ya Elimu Tanzania
(TET) kuwa na uwezo wa kuchapisha vitabu vyake nchini badala ya kutegemea
viwanda vya nje ya nchi.
Hayo yamesemwa terehe 14/05/2022 na Waziri wa
Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf Mkenda (Mb) wakati alipotembelea
viwanda vya uchapaji vy TET.
"Hapa lazima kuiwezesha TET ndani ya mwaka
mmoja iwe imepata mashine kubwa ya kuchapa na kutafuta tenda nafuu ya malighafi
ya karatasi kwa ajili ya uchapaji wa vitabu ili kuhakikisha inaongeza ajira kwa
watanzania kupitia viwanda hivyo" amesema Pro.Mkenda.
Hata hivyo, Prof. Mkenda amesema
serikali imedhamiria kuimarisha uchapishaji kwa kuiwezesha TET kupata karatasi
kwa bei nafuu, umeme wa uhakika na mashine kubwa ya kisasa ya uchapaji.
Pia aliielekeza TET kutumia wataalamu wote wa
nchini na wa nje ya nchi ili kuweza kufikia malengo katika ubora.
Aidha aliipongeza TET kwa kuanzisha mfumo wa kusoma
vitabu kwa mtandao (maktaba mtandao) na kusema kuwa utasaidia walimu na
wanafunzi kupata vitabu kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TET Dkt. Aneth Komba
amesema kuwa Kiwanda cha uchapaji cha Press A ni moja kati ya viwanda saba vya
taasisi hiyo na walikabidhiwa na wizara tangu mwaka 2019.
Ameeleza kuwa viwanda vya TET vinatumika kuchapa
kazi mbalimbali za Serikali na mashirika binafsi.