Uandaaji wa Mtaala hupitia hatua kadhaa na ni endelevu. Uandaaji huanza kwa kupitia maandiko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ili kupata mwelekeo wa mabadiliko ya elimu kitaifa na kimataifa. Mapendekezo na mahitaji ya elimu katika maandiko haya husaidia kuandaa zana za kuendesha tafiti kuhusu mitaala.
Tafiti huendeshwa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wazazi, wakufunzi, wahadhiri, waajiri, walimu, wakaguzi wa shule, wasimamizi wa elimu, watunga sera, wanafunzi, vyama vya kitaaluma, kitaalam na siasa, vyombo vya dini na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali.
Rasimu ya kwanza ya mtaala (draft) hutolewa na kujaribiwa shuleni au vyuoni ili kupata maoni, hatua ambayo hufuatiwa na uandaaji wa mitaala. Baada ya hapo,
wadau hupitishwa katika mtaala ili kutoa maoni kama yapo, na kama hakuna maoni ya ziada, mtaala huidhinishwa kwa ajili ya matumizi. Mtaala rasmi huchapwa pamoja na maandiko yanayotafsiri mitaala kama vile mihtasari na miongozo mingine kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wake.
Mtaala wa Elimu ni mwongozo mpana unaoweka viwango vya
utoaji elimu kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:
(i) Ujuzi watakaoujenga wanafunzi (competences) yaani maarifa (knowledge), stadi (skills) na mwelekeo (attitudes);
(ii) Njia za kufundishia na kujifunzia zitakazotumika katika utekelezaji wa mtaala
(pedagogical orientations);
(iii) Vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyohitajika;
(iv) Upimaji, ufuatiliaji na tathmini ya mtaala husika;
(v) Sifa za kitaaluma na kitaalamu za mwalimu atakayeuwezesha mtaala husika;
(vi) Miundombinu wezeshi (enabling infrastructure) kwa utekelezaji wa mtaala wenye ufanisi; na
(vii) Muda utakaotumika katika ufundishaji/utekelezaji wa mtaala.