WALIMU WASISITIZWA MAADILI KATIKA MAENEO YAO YA UTENDAJI

NAIBU Katibu Mkuu OR TAMISEMI Bw. Atupele Mwambene ametoa wito kwa walimu wa ajira mpya walioshiriki mafunzo maalumu ya Elimu ya Biashara na Amali kuzingatia maadili, nidhamu na moyo wa kujitolea katika maeneo yao ya utendaji.
Bw. Mwambene ametoa wito huo leo Juni 28, 2025 wakati akihitimisha mafunzo maalumu ya siku kumi kwa walimu wa ajira mpya wa somo la elimu ya biashara na Amali ambayo yaliyofungiwa Korogwe Mkoani Tanga.
"Nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa ualimu ni taaluma ya kipekee iliyojaa uzito wa kijamii na kiutaifa. Ni wito unaohitaji siyo tu maarifa na ujuzi, bali pia moyo wa kujitolea, nidhamu ya hali ya juu, na maadili thabiti ya kitaaluma." Amesema Bw. Mwambene.
Amesema, katika mazingira ya sasa ya mabadiliko ya Mitaala na mitazamo ya elimu, mwalimu anategemewa kuwa kiongozi wa maarifa, mlezi wa maadili, na mwezeshaji wa ujenzi wa umahiri kwa wanafunzi.
Aidha, Bw. Mwambene amewasihi walimu hao kuziishi kwa vitendo kanuni na taratibu za utumishi wa umma, huku akisisitiza juu ya uzalendo kuwa dira yao katika utendaji wao kwa kulenga siyo tu kufundisha, bali kulea na kuongoza kizazi cha sasa kuwa raia bora wa kesho.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema lengo la mafunzo ni kuwajengea walimu uelewa kuhusu taaluma ya Ualimu, uwezo wa kutumia mbinu stahiki za ufundishaji na ujifunzaji darasani, uandaaji wa masomo na kutoa ushauri wa kitaaluma na malezi kwa wanafunzi.
Sambamba na hayo Dkt. Komba ameeleza, walimu hao wamewezeshwa katika umahiri mahususi ili kuwajengea uelewa walimu hao kuhusu majukumu ya mwalimu katika utekelezaji wa Mtaala na masuala mengine ya kijamii katika maisha ya wanafunzi shuleni.
Amesema, maeneo mengine ambayo walimu hao wamewezeshwa ni kukuza uelewa kuhusu Mtaala na mihutasari ya Elimu ya Amali na biashara, kumudu mbinu mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji, kumudu mbinu za upimaji na tathmini.