SERIKALI KUINGIZA MASHINDANO YA STADI ZA UFUNDISHAJI KWA WALIMU KATIKA BAJETI KUU

Serikali imepanga kuingiza mashindano ya stadi za ufundishaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kwenye bajeti kuu ya taifa kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuyawezesha mashindano hayo kuwa endelevu.
Kwa sasa shindano hilo hayo linandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi (BOOST).
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi tuzo kwa washindi wa mashindano ya tatu kwa walimu wa msingi na ya kwanza kwa walimu wa sekondari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema ni wakati sasa kwa Serikali kuanza kuyawezesha mashindano hayo kifedha.
“Najua Benki ya Dunia mnaendelea kufadhili mashindano haya, lakini sasa ni wakati wa Serikali yetu kuanza kuyaingiza kwenye bajeti ili yawe endelevu. Naagiza maandalizi yaanze Julai 2025,” alisema Profesa Mkenda huku akimuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara kuanza maandalizi hayo.
Katika hafla hiyo, Profesa Mkenda alikabidhi zawadi kwa washindi wa kwanza, pili na tatu kwa masomo mbalimbali ikiwamo biolojia, fizikia, hisabati, sayansi na kemia huku akiwapongeza kwa ubunifu waliouonesha.
“Nawapongeza wote waliopata tuzo na wale wa nafasi ya nne hadi ya kumi waliopata vyeti na zawadi ya fedha. Ushindi huu uwe chachu ya kuendelea kuboresha mbinu za ufundishaji zinazolingana na mtaala mpya wa elimu,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa walimu si tu wanatoa elimu darasani bali pia hutoa malezi na mwelekeo kwa watoto wanaowafundisha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Aneth Komba alisema mashindano hayo yamekuwa yakifanyika kwa miaka mitatu mfululizo kwa walimu wa elimu ya awali na msingi, huku mwaka huu kwa mara ya kwanza yakijumuisha pia walimu wa sekondari.
Katika shule za msingi, walimu walishindana kwa kufundisha somo la sayansi kwa darasa la nne, huku kwa sekondari (Kidato cha Kwanza) walimu walishindana katika masomo ya kemia, fizikia, hisabati, Kiingereza na matumizi ya TEHAMA.
Kwa mujibu wa Kombo, jumla ya shule 184 kutoka wilaya zote nchini ziliwasilisha video za walimu wakifundisha stadi mbalimbali kati ya Machi na Aprili mwaka huu.
Baada ya video hizo kukaguliwa na majaji kwenye ngazi ya halmashauri, video bora 10 kutoka kila halmashauri zilipelekwa ngazi ya kanda ambapo video 1,840 zilichujwa na jopo la majaji wanane kutoka kila kanda.
Hatimaye video bora 10 kutoka kila kanda ziliwasilishwa kwa ajili ya mchujo wa kitaifa ambapo video 118 ziliingizwa kwenye Mfumo wa Taifa wa Kujifunza (National TIE Learning System) kwa uchambuzi zaidi na kupata washindi 44 waliotangazwa.
Mbali na mchujo huo wa video, walimu walifanya pia majaribio ya vitendo kwa kufundisha kwa dakika 15 (micro-teaching) ili kuthibitisha uhalisia wa stadi zao.
Katika upande wa zawadi, washindi wa kwanza walipokea Shilingi milioni nne kila mmoja, wa pili Shilingi milioni tatu , wa tatu Sh2.5 milioni na walioshika nafasi ya nne hadi ya kumi walipata cheti na Sh1 milioni kila mmoja. Aidha, video 15 bora zaidi zitaendelea kutumika kama rejea katika mafunzo kwa walimu wengine.
Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Gema Toddy aliwataka walimu washindi kuhakikisha maarifa waliyo nayo wanawapatia walimu wenzao.